Thursday, 12 January 2017

ZAMU YAO IMEKWISHA

Imeshatanda huzuni,wakenya tutaabani,
Mawakili wambioni,waangamia wendani,
Wasita mahakamani,mandamano barabarani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Hakika hatuna imani,na tume wanazobuni,
Kila siku hatuoni,faida zake nchini,
Mwishowe wanabaini,mwenye tarifa tokeni,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Na tazama na sioni,takoma maafa lini,
Najuliza akilini,taswira hapo mwanzoni,
Masheikh misikitini,waliwauwa jamani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Ninalipaza hewani,ninaogopa manani,
Binadamu takuthamini,uongo ukilongani,
Ukweli kifichuani,mitutu takupigani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Ulionalo machoni,kimya wao wakwambeni,
Bora wende marekani,gure kwenu kiamboni,
Taridhia maishani,kibadili usitizeni,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Wakutusaidia nani,fikapo mahakamani,
Mawakili wawatisheni,watiwapo kizimbani,
Hakika watawalani,hutafaa maishani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Nimefika ukingoni,najifungia chumbani,
Sitoki barabarani,watanandama nadhani,
Yaillah ya manani,bariki kenya amani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Ramadhan Mwaruwa Nyae
"Mti Mgumu"
Magongo_Mombasa.

No comments:

Post a Comment