Sunday, 8 January 2017

UPO UMRI

 











U’tulivu moyo wangu,sina mori ya madadi
Kupenda penda ukungu, sifanyi alimuradi
Nawatangazia gungu,wavuli m’nojinadi
Upo umri sahihi, umri wa kuaminika.
Umri unogao pungu,mbongo kutia juhudi
Kuposa kwa walimwengu,iwe kheri ya wahidi
Sitafanya wanguwangu,kisa mimi maridadi
Upo umri sahihi, umri wa kuaminika.
Mwimbe mnipe uchungu, wimbo kwangu ni zawadi
Imbeni fungu kwa fungu,sifa zote msawidi
Siwezi kumla changu,chuchunge nimekaidi
Upo umri sahihi, umri wa kuniamini.
Si mlamba mla dengu, sili choroko mahindi
Sitegeki kwa majungu, wala mitego ya jadi
Mi mwenda juu kipungu,kurejea naradidi
Nasema upo umri, umri wa kuaminika
© 2016,Na Innocent Zephania

No comments:

Post a Comment