KITENDAWILI
Kitendawili natega, wateguzi tegueni,
Njiwa niliyemfuga, sitomla asilani,
Ingawa kanivuruga, kunitia matatani,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Njiwa niliyemfuga, sitomla asilani,
Ingawa kanivuruga, kunitia matatani,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Hutembea kwa madaha, na mbawa huziachia,
Nisijepata fedheha, wangu ndege kujilia,
Nabakia ni kihaha, sijue pakushika,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Nisijepata fedheha, wangu ndege kujilia,
Nabakia ni kihaha, sijue pakushika,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Siupati usingizi, kutwa nakesha nahaha,
Ninamuomba mwenyezi, niondolee karaha,
Niuone upuuzi, nisijepata fedheha,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Ninamuomba mwenyezi, niondolee karaha,
Niuone upuuzi, nisijepata fedheha,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Miti yote nitakwea, wa nyumbani tanishinda,
Wahenga waliomea, usemi waliuunda,
Kwa wote walozoea, njiwa wao kuwapenda,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Wahenga waliomea, usemi waliuunda,
Kwa wote walozoea, njiwa wao kuwapenda,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Ngekuwa wa bwana Juma, ningemla kwa miluzi,
Nisingepata tuhuma, na wala kipingamizi,
Ningeenda kiheshima, kuwajulisha walezi,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Nisingepata tuhuma, na wala kipingamizi,
Ningeenda kiheshima, kuwajulisha walezi,
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Kufuga sasa ni basi, sijepata vishawishi,
Niepuke usabasi, wa ndugu wenye utashi,
Uniondoke uasi, ili niweze kuishi.
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Niepuke usabasi, wa ndugu wenye utashi,
Uniondoke uasi, ili niweze kuishi.
Wateguzi tegueni, kishindwa nipeni mji.
Siye njiwa wa tunduni, yafaa kuwaambia.
Wala yule wa porini, na hili kuzingatia,
Iwaingie kilini, na jibu kunipatia,
Wateguzi tegueni,kishindwa nipeni mji.
Wala yule wa porini, na hili kuzingatia,
Iwaingie kilini, na jibu kunipatia,
Wateguzi tegueni,kishindwa nipeni mji.
Tamati nimefikia, wateguzi tegueni,
Maize mlobobea, kwa kirefu fikirini,
Sahihi kunipatia, majibu yenye thamani,
Wateguzi tegueni,kishindwa nipeni mji.
Maize mlobobea, kwa kirefu fikirini,
Sahihi kunipatia, majibu yenye thamani,
Wateguzi tegueni,kishindwa nipeni mji.
No comments:
Post a Comment