Wednesday, 11 January 2017

SIPONSA














Siyo yule wa zamani,mke niliyemjua
Ana mambo ya kigeni,Makini anizingua
Hakukaliki nyumbani,majonzi amenitia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Nanena pasi utani,wala kumsingizia
Amekuwa ja mhuni,wa kiburi kujitia
Ni mbishi kila fani,hana analosikia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Hapiki tena jikoni,akiri kajichokea
Adai moshi wa kuni,kashindwa kuvumilia
Heri niende sokoni,meko kumnunulia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Mchicha atema chini,sauti kinipazia
Eti nifike dukani,na piza kumletea
Mambo haya mambo gani,ni nani kamchochea?
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Ana rangi mdomoni,michoro kajichorea
Puani ana vipini,wanja macho ipo pia
Nguo zake za thamani,ni nani kagharamia?
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Kitoka huja jioni,bila katu kunambia
Kifika huyo simuni,mwenyewe ajichekea
Si siri nina mgeni,kiumbe nisomjua
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Lugha yake nayo gani,mwenzenu sijatambua
Alo mfunza ni nani,nawaza na kuwazua
Tena alonga na nani,hilo moja kabania
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Siyo mwingi wa uneni,kinena anizomea
Hunibeza mtaani,aibu ananitia
Imi dume barazani,ila kwangu ninajifia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Ana tungo za kubuni,na safari kila saa
Wikendi haji nyumbani,sherehe kamzidia
Ni heri hapo zamani,ukapera kanifaa
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Mnifaeni wandani,si siri ninaumia
Kageuka hayawani,siwezi msongelea
Nachezwa mie jamani,serikali saidia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Msafiri Makini

No comments:

Post a Comment