Monday, 9 January 2017

NIDAI NINGALI HAI














Afiya yangu si nzuri,yanihasiri maini,
Imenizidi nasuri,guu langu taabani,
Nachungulia kaburi,kupona kwangu sidhani,
Nidai ningali hai,nikifa msinidai.
Mwilini zangu ateri,zimeziba mishipani,
Damu hainayo kheri,yakwamakwama ndiyani,
Mepungukiwa kahari,nitaaga karibuni,
Nidai ningali hai,nikifa msinidai.
Tangia alfajiri,nagaagaa yakini,
Hadi sasa adhuhuri,ndivyo tena kitandani,
Ikijiri alasiri,nitawapa buriani,
Nidai ningali hai,nikifa msinidai.
Imedhihiri shahiri,sitakuwa aswilani,
Makao yangu kaburi,mle nitakuwa ndani,
Senti zenu kwa hiari,niwape harakisheni,
Nidai ningali hai,nikifa msinidai.
Kunao wale ayari,watayaghuri madeni,
Wanze kudai kwa ari,kufilisi masikini,
Ndiposa nimehubiri,kuweka haya bayani,
Nidai ningali hai,nikifa msinidai.
Katika yangu safari,sitaki enda na deni,
Bora nilipe fakiri,nituame kwa amani,
Aila yangu dahari,iwe nayo afueni,
Nidai ningali hai,nikifa msinidai.
Amos O. Nyakundi.
"Muongozo Madhubuti"
Kisii,Marani@Kegogi.

No comments:

Post a Comment