Nyumba ni changa ingali, ni juzi bati metiwa
Latoa mwanga mkali, kunguni wanaunguwa
"Mavumbi" kila mahali, "mashimo" yafumuliwa
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Wachekelea "walali", walau wanapumuwa
Wasojiweza kwa hali, "Pole" wamezishapewa
Walojazana kwa Meli, Mafuta zimeshatiwa
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Upike mkavu "wali", maharage taletewa
Japo mezani ni mbali, vinono tumetengewa
Nyuki wapenda asali, "masega" yaondolewa
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Tuanze kwa kutambaa, tufike na ukomavu
Tujifunge vitambaa, ngozi tupake majivu
Yakiyoyoma masaa, tuvae uvumilivu
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Yule aliyetuzaa, ameshamea mizizi
Walezi wakalemaa, kutufungia hirizi
Wa "chini" tukadumaa, kwa njaa na unyafuzi
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Ni mbali tumetokea, twaonekana wa juzi
Ruksa tulipokea, yakashiba manyakuzi
Tukashindwa kusogea, kazi kupiga miluzi
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Kuinowa yetu timu, Beni "safi" straika
Kaja na wake wazimu, mwanzoni palichimbika
Alipo "shibisha" hamu, timu choka nyakanyaka
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Akaja "Shemeji" ndani, kang'owa ya Goli Miti
Tukaachwa uwanjani, tunaikagua Neti
Tukimsifu Kinywani, "Bingwa" kupiga Penati
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Juzi juzi tumezaa, chanda tulichokitaka
Kisopenda "ujamaa", mwendo mchakamchaka
Yani ni la moto kaa, kinavyofyeka vichaka
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Tutambae mbele twende, tukomae tufikapo
Acha mwanzoni tukonde, ngali kibichi kiapo
Msingi kwenye mabonde, tusilie aendapo
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Tutakomaa najua, ziendavyo siku mbele
Makubwa "tukitumbua",havina shida vipele
Achomaye vitumbua, sasa auze mchele
Tuanze kwa kutambaa,tufike tumekomaa
Kahabi wa Isangula
Malenga wa Ngumbalu