Monday, 16 January 2017

KISA CHA NGARIBA












Ngariba ni maarufu
Alitisha ka harufu
Alikomba masurufu
Ya noti na misarafu
"Vipembe" alivikata
Mabinti kuwakeketa
Walimwita katakata
Sifaze zikatapata
Du nikupe kisa hiki
Siku alipofariki
Waosha wakahakiki
Hakuwahi kushiriki
Hakuwahi tohariwa
Waosha waligunduwa
Maiti lipofunuwa
Wakabaki kuduwaa!

Sunday, 15 January 2017

MWINGA KIKOROMEO

Mwinga wetu mamboleo, mwinga semi nyodo nyundwa
Mwinga domo kisemeo, kisa mwanetu kapendwa
Mwinga kinywa kichembeo, wakweze kutwa kusundwa
Mwinga ni kikoromeo, mwinga huyu hakufundwa!
Mwinga huyu shaitwani, mwinga binti ibilisi
Achukiaye jikoni, mwinga mpenda Chipsi
Asoficha maungoni, mwinga zi wazi hipsi
Mwinga ni kikoromeo, mwinga huyu hakufundwa!
Mwinga kutwa fesibuku, mambo tachitachi ati
Mwinga si wa bukubuku, kumi kumi zake noti
Asopenda chukuchuku, mwinga ni kuku rosti
Mwinga ni kikoromeo, mwinga huyu hakufundwa!
Mwinga ni nusu adabu, ni kichomi cha mapafu
Husonya hata mababu, wakwe zake ni wachafu
Mwinga haoni aibu, kufanya yanayokifu
Mwinga ni kikoromeo, mwinga huyu hakufundwa!
Mwinga huyu katushinda, tumechoka vumilia
Vile yeye kampenda, mwanetu twamlilia
Mwinga huyu ni kidonda, dawa kisichosikia
Mwinga ni kikoromeo, mwinga huyu hakufundwa!

Saturday, 14 January 2017

TUANZE KWA KUTAMBAA, TUFIKE TUMEKOMAA














Msuba nipo safari, mbali nikitembelea
Nimezipata habari, "ujenzi" waendelea
Tulivyoboresha dari, 'mijipopo" yaelea
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Nyumba ni changa ingali, ni juzi bati metiwa
Latoa mwanga mkali, kunguni wanaunguwa
"Mavumbi" kila mahali, "mashimo" yafumuliwa
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Wachekelea "walali", walau wanapumuwa
Wasojiweza kwa hali, "Pole" wamezishapewa
Walojazana kwa Meli, Mafuta zimeshatiwa
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Upike mkavu "wali", maharage taletewa
Japo mezani ni mbali, vinono tumetengewa
Nyuki wapenda asali, "masega" yaondolewa
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Tuanze kwa kutambaa, tufike na ukomavu
Tujifunge vitambaa, ngozi tupake majivu
Yakiyoyoma masaa, tuvae uvumilivu
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Yule aliyetuzaa, ameshamea mizizi
Walezi wakalemaa, kutufungia hirizi
Wa "chini" tukadumaa, kwa njaa na unyafuzi
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Ni mbali tumetokea, twaonekana wa juzi
Ruksa tulipokea, yakashiba manyakuzi
Tukashindwa kusogea, kazi kupiga miluzi
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Kuinowa yetu timu, Beni "safi" straika
Kaja na wake wazimu, mwanzoni palichimbika
Alipo "shibisha" hamu, timu choka nyakanyaka
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Akaja "Shemeji" ndani, kang'owa ya Goli Miti
Tukaachwa uwanjani, tunaikagua Neti
Tukimsifu Kinywani, "Bingwa" kupiga Penati
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Juzi juzi tumezaa, chanda tulichokitaka
Kisopenda "ujamaa", mwendo mchakamchaka
Yani ni la moto kaa, kinavyofyeka vichaka
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Tutambae mbele twende, tukomae tufikapo
Acha mwanzoni tukonde, ngali kibichi kiapo
Msingi kwenye mabonde, tusilie aendapo
Tuanze kwa kutambaa, tufike tumekomaa
Tutakomaa najua, ziendavyo siku mbele
Makubwa "tukitumbua",havina shida vipele
Achomaye vitumbua, sasa auze mchele
Tuanze kwa kutambaa,tufike tumekomaa
Kahabi wa Isangula
Malenga wa Ngumbalu

Friday, 13 January 2017

JIRANI












Unisamehe jirani, imenibidi niseme,
Sikutaka aswilani, ila nataka ukome,
Unitiapo machoni, nilazima uiname, 
Yawaje hivyo jamani, ilhali rinda fupi?
Nipitapo varandani, yawaje usisimame?
Waitandaza ramani, unataka niisome,
Tabasamu mudomoni, sikujua paka shume,
Yawaje hivyo jamani, ilhali rinda fupi?
Benson Nyale
©2017

Thursday, 12 January 2017

NISHAPENDWA, KUPENDA TENA SIWEZI















kupendwa nilishapendwa, kupenda tena siwezi.
Mapendoni nikalindwa, 'sinitukuwe jambazi.
Na kurandwa ninarandwa, na wangu alo mjuzi. 
Nishampata azizi, tena sitaki kupendwa.
Mi si wakupindwapindwa, natangaza waziwazi .
Maudhiko nijetendwa, kwa mitego ya bazazi.
Kwani mtendi katendwa, mida yile chipukizi.
Nimetegwa mteguzi, na nyumbani nikatindwa.
Kiwa kukandwa nakandwa, maungoni kwa henezi.
Mahabani nikafundwa, kwa yake mema malezi.
Ngalikuwa ungashindwa, manake we we huniwezi.
Nishapata wa saizi, ungali wa andwa andwa.
Na usije ukapandwa, na mori wa sisimizi.
Mtimani ukarindwa, na hasira za mkizi.
Ukakuwa umegandwa, na yangu masimulizi.
Hivo kuwa msikizi, phibbiyanni nishapendwa.
Malenga mlezi
Phibbian Muthama
(c)2016

ZAMU YAO IMEKWISHA














Imeshatanda huzuni,wakenya tutaabani,
Mawakili wambioni,waangamia wendani,
Wasita mahakamani,mandamano barabarani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Hakika hatuna imani,na tume wanazobuni,
Kila siku hatuoni,faida zake nchini,
Mwishowe wanabaini,mwenye tarifa tokeni,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Na tazama na sioni,takoma maafa lini,
Najuliza akilini,taswira hapo mwanzoni,
Masheikh misikitini,waliwauwa jamani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Ninalipaza hewani,ninaogopa manani,
Binadamu takuthamini,uongo ukilongani,
Ukweli kifichuani,mitutu takupigani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Ulionalo machoni,kimya wao wakwambeni,
Bora wende marekani,gure kwenu kiamboni,
Taridhia maishani,kibadili usitizeni,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Wakutusaidia nani,fikapo mahakamani,
Mawakili wawatisheni,watiwapo kizimbani,
Hakika watawalani,hutafaa maishani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Nimefika ukingoni,najifungia chumbani,
Sitoki barabarani,watanandama nadhani,
Yaillah ya manani,bariki kenya amani,
Zamu masheikh mekwisha,kilio kwa mawakili.
Ramadhan Mwaruwa Nyae
"Mti Mgumu"
Magongo_Mombasa.

Wednesday, 11 January 2017

SIPONSA














Siyo yule wa zamani,mke niliyemjua
Ana mambo ya kigeni,Makini anizingua
Hakukaliki nyumbani,majonzi amenitia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Nanena pasi utani,wala kumsingizia
Amekuwa ja mhuni,wa kiburi kujitia
Ni mbishi kila fani,hana analosikia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Hapiki tena jikoni,akiri kajichokea
Adai moshi wa kuni,kashindwa kuvumilia
Heri niende sokoni,meko kumnunulia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Mchicha atema chini,sauti kinipazia
Eti nifike dukani,na piza kumletea
Mambo haya mambo gani,ni nani kamchochea?
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Ana rangi mdomoni,michoro kajichorea
Puani ana vipini,wanja macho ipo pia
Nguo zake za thamani,ni nani kagharamia?
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Kitoka huja jioni,bila katu kunambia
Kifika huyo simuni,mwenyewe ajichekea
Si siri nina mgeni,kiumbe nisomjua
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Lugha yake nayo gani,mwenzenu sijatambua
Alo mfunza ni nani,nawaza na kuwazua
Tena alonga na nani,hilo moja kabania
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Siyo mwingi wa uneni,kinena anizomea
Hunibeza mtaani,aibu ananitia
Imi dume barazani,ila kwangu ninajifia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Ana tungo za kubuni,na safari kila saa
Wikendi haji nyumbani,sherehe kamzidia
Ni heri hapo zamani,ukapera kanifaa
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Mnifaeni wandani,si siri ninaumia
Kageuka hayawani,siwezi msongelea
Nachezwa mie jamani,serikali saidia
Wanjiku kabadilika,lazima ana siponsa
Msafiri Makini