Monday, 23 November 2015

NANI NADHIFU



Msafiri napata safari, neno maana kulitafutia
Kutembea kila mandhari,tanzania hadi India
Ndege hata gari, bila hofu najipandia
machache yanipa tahayari,makubwa napata shangalia
Hakuna katu nadhifu,Mola yeye pekee

Sasa nachambua majibu,niliyopata kule safarini
Nakupeni wangu maswahibu,shuleni na mitaani
Sizidishi nikaja haribu,niliyopata kule mafichoni
kusema kweli thawabu,hujazwa tele thamani
Hakuna katu nadhifu, Mola yeye pekee

Kalamu ikiwa nene,muandiko huwa tafauti
Wanaume waringia wanne,wakikerwa huandika cheti
Wataka shamba wavune,bila kupalilia mti
Kuchezesha na sebene,mafunzo yale karati
Hakuna katu nadhifu, Mola yeye pekee

Waume wengine wajisahau,kurudi nyumbani usiku
Wake zao kuwadharau,michepuko wala kuku
wakirudi wajawa nahau, hawawezi kula daku
Kuwaita paka nyau,kugusana tena marufuku
Hakuna katu nadhifu,Mola yeye pekee

Kasheshe kina mama, wao wametia nukta
Wamesahau kivazi bahama,mjini kitop bukta
Hakuna tena kilema,fesheni kupanda ukutana
Ukipitwa na sinema,mitaani dhahiri utakuta
Hakuna katu Nadhifu, Mola yeye pekee

Jaribu kumuweka ndani, utaona adha yake
Wengine watoka ndoani,kuonjesha jirani zake
Anampenda yule wa zamani,huwezi mfanya aridhike
Talaka ipo mdomoni,huo Wimbo wake.
Hakuna katu nadhifu,Mola yeye pelee

Narudi kwako hadhira,usihukumu mtu mapungufu
Tuombe nasi nusura,yasitupate hayo machafu
Tujilinde na madhara,penzi lisipate Uhalifu
Tuchukizwe na hasira, Ndoa tusije zihalifu.
Hakuna katu Nadhifu,Mola yeye pekee


Sunday, 22 November 2015

MASHAIRI YASO VINA!


Mtunzi nimechutama,kusoma yasosomeka.
Imebidi kulalama,na kalamu kuishika.
Niwajuze himahima,niache kusononeka.
Mashairi yaso vina,ladha take hupotea.
Ladha take hupoteya,mashairi yaso vina.
Msomi huwayawaya,hulisoma akinuna.
Pia huliita baya,hamu fahamu hakuna.
Mashairi yaso vina,ladha yake hupotea.
Likifwatia urari,vina viwe mufatano.
Vina vikuwe chanjari,shairi lisewe ngano.
Lipangike kwa uzuri,tungo ikawe mfano.
Mashairi yaso vina,ladha yake hupotea.
Kwa langu hili shairi,mfano nitaangaza.
Msome na mfikiri,muone niloliwaza.
Mwone Halina fahari,lenyewe linajikwaza.
Mashairi yaso vina,ladha yake hupotea.
Hapa vina siviweki,tofauti ioneni.
Halipendezi machoni,ubeti una kasoro.
Urari haupo on a,linaudhi kilisoma.
Mashairi yaso vina,ladha yake hupotea.
Ubeti huo someni,urari haupo ndani.
Ladha haipo wendani,KI NI na tazameni.
Hitilafu mesheheni,Ni To na Ma oneni.
Mashairi yaso vina,ladha yake hupotea.
Nimewajuza wandani,yaso vina tambueni.
Mkisoma hazarani,yanazua ubishani.
Husumbua kiyaghani,furaha huwa huzuni.
Mashairi yaso vina,ladha yake hupotea.
Utunzi wa.
Sauti ya babu.
Mstahiki Zack.

Sunday, 6 September 2015

AINA ZA USHAIRI (BAHARI)


Bahari; hii ni aina mahususi ya  ushairi yenye sifa fulani kiumbo na pengine hata kimaudhui na kimatumizi na zinazoipambanua na aina nyingine ya ushairi.
S.A Kibao (2003)  anasema, ushairi wa Kiswahili umegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni: shairi, utenzi na ngonjeara. Anaendelea kusema, aina zote hizi kanuni zake ni za pamoja isipokuwa utenzi ambao una mpangilio wa namna ya pekee.
S. Robert na Amri Abeid (1954)  wanasema zipo bahari tatu tu za ushairi nazo ni:wimbo, shairi na utenzi.
A.S. Nabhany na wenzake wameainisha bahari 13 za ushairi na kusema kuwa utungo wowote lazima uingie katika bahari mojawapo. Bahari hizo ni hizi zifuatazo:
1.      Ushairi; Ni utenzi wenye mishororo minne na vipande  viwili kila msitari. Kila mstari una mizani 16 na kila kipande kina mizani 8. Maudhui yake yanatokana na jambo lolote lile analoliona mtunzi.
2.      Wimbo; Ni utungo wenye mishororo mitatu kila ubeti na kila mshororo una vipande viwili. Nyimbo nyingi huongelea mapenzi.
3.      Tenzi; Ni utungo wenye vipande vine katika kila ubeti na vina hubadilika kila ubeti isipokuwa kipande cha mwisho. Tenzi nyingi zina mizani nane kila mshororo na nyingine zina mizani 11 na zingine 10.
4.      Inkshafi/Duramandhuma; Imepata jina lake kutokana na utenzi wa Aliinkshafi. Tenzi hizi zina maadili ya kidini japokuwa maudhui yake yanaweza kutumika katika maadili ya kidunia. Kila ubeti una mishororo minne na kila mshororo una mizani 11.
5.      Ukawafi; Hili ni shairi lenye mishororo mitatu au zaidi katika kila ubeti na vipande vitatu katika kila mshororo. Mizani zinaweza zikatofautiana au zikawa sawa.
6.      Wajiwaji/Takhimisa; Una mishororo mitano kila ubeti na mizanai 15 kila mshororo na vipande vitatu katika kila mshororo vina muundo wa mizani 6, 4, 5. Maudhui yake ni ya kidini au kiamisha kwa ujumla, mfano Takhimisa ya Liongo  na tenzi ya Inkshafi.
7.      Hamziya; lipata jina lake kutokana na kaswida ya Hamziya ambao ni utenzi wa kiarabu. Mishororo ya Hamziya ina vipande 3 vya mizani 5, 4, 6
8.      Tiyani-Fatiha;   Ni ushairi wa kidini wa kuomba toba, una mishororo 9 kila ubeti ambayo huweza kutofautiana kwa urefu/mizani.
9.      Utumbuizo; Haina idadi kamili ya mishororo na mizani, urefu wa mstari au mshororo hutegemea pumzi aliyonayo mwimbaji na lengo lake; mfano ni nyimbo za Liyongo kuna tumbuizo.
10.  Wawe; Ni ushairi au wimbo wa kilimo, huimbwa wakati wa kulima au kupanda.
11.  Kimai; Inahusu shughuli za majini, ni bahari ya wavuvi na mabaharia. Idadi ya mishororo na vina si lazima.
12.  Zivindo; Ni ushairi unaofafanua maana za maneno; na kazi yake ni kujifunza lugha na mkuhifadhi lugha.
Mfano: Kata ni kata ya nyoka
             Au kata ya nyweleni
             Kata ya tweka, bandikwayo kichwani
13.  Sama; Neno ‘sama’ ni mahadhi au sauti, hivyo bahari hii hukusanya washairi wote wenye kufuata mahadhi ya kigeni.

Tuesday, 1 September 2015

MAMBA NA KIBOKO


Nimechoka sokomoko, mkulima wa Mnavu
Kila siku chokochoko,ninapofata unyevu
Leo naketi kitako,kuteta na wamabavu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?


Mimi langu nung’uniko,ni tabia yenu mbovu
Mwaligeuza tandiko,shamba langu endelevu
Sasa mwaninyima soko,kwa hayo yenu maovu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

Mwafahamika si koko, bali viumbe tulivu
Kajibebea ujiko, maji ndo chenu kitovu
Tulieni huko huko,mkiupata uchovu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

Menikwangua ugoko,nusu niwe mlemavu
Nawaomba badiliko,bado mnaona wivu
Hili ndo lenu anguko,takaloleta kivumvu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

Ngoja nikivute kiko,kusudi nipate nguvu
Niandae mlipuko,wa vyuma vyangu chakavu
Tawafanya rikoriko,nijipatie wagivu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

Wenzangu nipeni heko,mkulima si pumbavu
Bora kusema kuliko,kuonekana mvivu
Kama kwenu ni kicheko,kwangu mimi maumivu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

©2014 Na Innocent Zephania.

DENGU

Naona nyote mwang'ara, niwekeni muangani,
Nijitokeze jahara, ya sawa niyabaini,
Sina budi imi jura, kuwauza kilingeni,
Kwa ndimi zenu na sura, dengu ni za rangi gani?


Kwa nyugwe nawazingira, mtamke kwa lisani,
Nyote wa pwani na bara, mlotanganyika ndani,
Nizingapo sina dira, akilini na matoni,
Kwa ndimi zenu na sura, dengu ni za rangi gani?

Msifate ya bendera, pepo zenu zifanani,
Tamkeni bila jera, kwa aswili zenye tani,
Tamka msi izara, tata hini tatueni,
Kwa ndimi zenu na sura, dengu ni za rangi gani?

Zitieni ndimi ghera, mtamke ranji hini,
Nafaka yenye ubora, wa zihi za muilini,
Tena haina madhara, ni ya aswili shambani,
Kwa ndimi zenu na sura, de ngu ni za rangi gani?

Mafaswiha wa busara, zuo zenu angazeni,
Hayano kwenu ibura, mliokwima mbeeni,
Hela msiete tara, ranji hini tujuzeni,
Kwa ndimi zenu na sura, dengu ni za rangi gani?

Yakubu Ngumbao Julius
''moto wa kifuu''
4-8-2015
Nairobi- Kenya

UJANA


Maisha ni neno pana, Maanae sifukui
Mapacha weza fanana, Kwenye kiza huwajui
Hodihodi waungwana, Nivalisheni kikoi
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai


Ya jana ndo ya ujana, Mzee sijisumbui
Hapo maisha hubana, Na kuhisi hupumui
Shida zikafumukana, Mithili utandubui
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai

Starehe za ujana, Mengi hauyang’amui
Hasa upatapo bwana, Hufanya hujitambui
Ila mtapotengana, Maziwa taona tui
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai

Ujana kubwa hazina, Kama mlima sinai
Ukicheza danadana, Hilo kosa la jinai
Mwisho chochote hakuna, Uzee utakudai
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai

Leo ilikua jana, Wakati hauzubai
Tumia vyema ujana, Dhalili nakupa rai
Ujana ulevi bwana, Uzee ni jitmai
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai

Tamati ninafikia, Mbele tena sisogei
Vyema ujana tumia, Afya isikulaghai
Usije ukajutia, Uzee ukisabai
Ya jana mpe kijana , Uzee asitumai

LIMETUNGWA NA NASRI KIONE
0752300012 nasriibrahimu@gmail.com
(FB) TUNGO ZENYE ULIMBO

Thursday, 28 May 2015

OA

OA

Oa nakwambia kaka, singoje kunasiwa,
Oa yapita miaka, ‘site ngoma kupigiwa,
Oa ‘epuke kumaka, usije kulia ngowa,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.


Oa walio na maadili, so sura kuangaliya,
Oa wenye uhiimili, epuka wenye umbeya,
Oa wenye muamali, nyumbani watatuliya,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa hata wa mjini, bora kwa mda kumjuwa
Oa aliye wa kuamini, sumu sije kutiliwa,
Oa kaka kwa makini, sije sema “ningejuwa,”
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa ukiwa kijana, ndoa mapema ku’ngiya,
Oa ulipe dhamana, vyema watoto kuleya,
Oa wajua ujana, ni moshi wa kufukiya,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa wakujitafutiya, nasaha yangu natowa,
Oa uliye dhamiriya, sio mke kuletewa,
Oa tena nakwambiya, sitake wakunadiwa,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa uepuke upweke, na msongo kujitiya,
Oa ukiwa na makeke, kabla uzee kuingiya,
Oa uhuni sitake, sije kufa kwa uthiya,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa upate mwandani, kwa ubani kufukiwa,
Oa kitu cha dhamani, kinda bata na njiwa,
Oa na umweke ndani, waambiwe umeowa,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

©2014 WILLY LUSIGE
"Malenga wa kuvizia"

SINA HAKI YA KUPENDA

SINA HAKI YA KUPENDA

Kwako mola shitakia, Dua zangu pokea,
Binadamu wachekea, umbile langu sikia,
Ufupi lonipatia, kunitusi wanambia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Ni majuzi litokea, kisa kilonifikia,
Mrembo alinambia, huba kwangu futilia,
 Weye nyundo sikia, kukupenda najutia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Mie ninazo hisia, kama warefu sikia,
Yarabi hakukosea, ufupi nakunumbia,
Mola unampangia, maumbile kashifia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Swali ninaulizia, malenga kunijibia,
Moyoni ninaumia, ninashindwa vumilia,
Matamshi lonambia, maulana nakwachia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Miaka imewadia, ninyi nyundo kubakia,
Twiga wameshaingia, naona mutaumia,
Ninaanza kujutia, ufupi livyonijia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Sio ninakwingilia, ukanamba nimevia,
Kiapo nakuapia, uliyanena sikia,
Rafiki sitokataa, japo mawi linambia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Tamati Rama nalia, machozi yabubujia,
Nenda kwetu kutulia, dhiki imenivamia,
Yaillah yajalia, Jalie alo sawia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

RAMADHAN MWARUWA NYAE
“MALENGA MTI MGUMU”
MENZAMWENYE – LUNGALUNGA.