Sunday, 6 September 2015

AINA ZA USHAIRI (BAHARI)


Bahari; hii ni aina mahususi ya  ushairi yenye sifa fulani kiumbo na pengine hata kimaudhui na kimatumizi na zinazoipambanua na aina nyingine ya ushairi.
S.A Kibao (2003)  anasema, ushairi wa Kiswahili umegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni: shairi, utenzi na ngonjeara. Anaendelea kusema, aina zote hizi kanuni zake ni za pamoja isipokuwa utenzi ambao una mpangilio wa namna ya pekee.
S. Robert na Amri Abeid (1954)  wanasema zipo bahari tatu tu za ushairi nazo ni:wimbo, shairi na utenzi.
A.S. Nabhany na wenzake wameainisha bahari 13 za ushairi na kusema kuwa utungo wowote lazima uingie katika bahari mojawapo. Bahari hizo ni hizi zifuatazo:
1.      Ushairi; Ni utenzi wenye mishororo minne na vipande  viwili kila msitari. Kila mstari una mizani 16 na kila kipande kina mizani 8. Maudhui yake yanatokana na jambo lolote lile analoliona mtunzi.
2.      Wimbo; Ni utungo wenye mishororo mitatu kila ubeti na kila mshororo una vipande viwili. Nyimbo nyingi huongelea mapenzi.
3.      Tenzi; Ni utungo wenye vipande vine katika kila ubeti na vina hubadilika kila ubeti isipokuwa kipande cha mwisho. Tenzi nyingi zina mizani nane kila mshororo na nyingine zina mizani 11 na zingine 10.
4.      Inkshafi/Duramandhuma; Imepata jina lake kutokana na utenzi wa Aliinkshafi. Tenzi hizi zina maadili ya kidini japokuwa maudhui yake yanaweza kutumika katika maadili ya kidunia. Kila ubeti una mishororo minne na kila mshororo una mizani 11.
5.      Ukawafi; Hili ni shairi lenye mishororo mitatu au zaidi katika kila ubeti na vipande vitatu katika kila mshororo. Mizani zinaweza zikatofautiana au zikawa sawa.
6.      Wajiwaji/Takhimisa; Una mishororo mitano kila ubeti na mizanai 15 kila mshororo na vipande vitatu katika kila mshororo vina muundo wa mizani 6, 4, 5. Maudhui yake ni ya kidini au kiamisha kwa ujumla, mfano Takhimisa ya Liongo  na tenzi ya Inkshafi.
7.      Hamziya; lipata jina lake kutokana na kaswida ya Hamziya ambao ni utenzi wa kiarabu. Mishororo ya Hamziya ina vipande 3 vya mizani 5, 4, 6
8.      Tiyani-Fatiha;   Ni ushairi wa kidini wa kuomba toba, una mishororo 9 kila ubeti ambayo huweza kutofautiana kwa urefu/mizani.
9.      Utumbuizo; Haina idadi kamili ya mishororo na mizani, urefu wa mstari au mshororo hutegemea pumzi aliyonayo mwimbaji na lengo lake; mfano ni nyimbo za Liyongo kuna tumbuizo.
10.  Wawe; Ni ushairi au wimbo wa kilimo, huimbwa wakati wa kulima au kupanda.
11.  Kimai; Inahusu shughuli za majini, ni bahari ya wavuvi na mabaharia. Idadi ya mishororo na vina si lazima.
12.  Zivindo; Ni ushairi unaofafanua maana za maneno; na kazi yake ni kujifunza lugha na mkuhifadhi lugha.
Mfano: Kata ni kata ya nyoka
             Au kata ya nyweleni
             Kata ya tweka, bandikwayo kichwani
13.  Sama; Neno ‘sama’ ni mahadhi au sauti, hivyo bahari hii hukusanya washairi wote wenye kufuata mahadhi ya kigeni.

Tuesday, 1 September 2015

MAMBA NA KIBOKO


Nimechoka sokomoko, mkulima wa Mnavu
Kila siku chokochoko,ninapofata unyevu
Leo naketi kitako,kuteta na wamabavu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?


Mimi langu nung’uniko,ni tabia yenu mbovu
Mwaligeuza tandiko,shamba langu endelevu
Sasa mwaninyima soko,kwa hayo yenu maovu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

Mwafahamika si koko, bali viumbe tulivu
Kajibebea ujiko, maji ndo chenu kitovu
Tulieni huko huko,mkiupata uchovu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

Menikwangua ugoko,nusu niwe mlemavu
Nawaomba badiliko,bado mnaona wivu
Hili ndo lenu anguko,takaloleta kivumvu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

Ngoja nikivute kiko,kusudi nipate nguvu
Niandae mlipuko,wa vyuma vyangu chakavu
Tawafanya rikoriko,nijipatie wagivu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

Wenzangu nipeni heko,mkulima si pumbavu
Bora kusema kuliko,kuonekana mvivu
Kama kwenu ni kicheko,kwangu mimi maumivu
Mbona mamba na kiboko,mwaniwinda nchi kavu?

©2014 Na Innocent Zephania.

DENGU

Naona nyote mwang'ara, niwekeni muangani,
Nijitokeze jahara, ya sawa niyabaini,
Sina budi imi jura, kuwauza kilingeni,
Kwa ndimi zenu na sura, dengu ni za rangi gani?


Kwa nyugwe nawazingira, mtamke kwa lisani,
Nyote wa pwani na bara, mlotanganyika ndani,
Nizingapo sina dira, akilini na matoni,
Kwa ndimi zenu na sura, dengu ni za rangi gani?

Msifate ya bendera, pepo zenu zifanani,
Tamkeni bila jera, kwa aswili zenye tani,
Tamka msi izara, tata hini tatueni,
Kwa ndimi zenu na sura, dengu ni za rangi gani?

Zitieni ndimi ghera, mtamke ranji hini,
Nafaka yenye ubora, wa zihi za muilini,
Tena haina madhara, ni ya aswili shambani,
Kwa ndimi zenu na sura, de ngu ni za rangi gani?

Mafaswiha wa busara, zuo zenu angazeni,
Hayano kwenu ibura, mliokwima mbeeni,
Hela msiete tara, ranji hini tujuzeni,
Kwa ndimi zenu na sura, dengu ni za rangi gani?

Yakubu Ngumbao Julius
''moto wa kifuu''
4-8-2015
Nairobi- Kenya

UJANA


Maisha ni neno pana, Maanae sifukui
Mapacha weza fanana, Kwenye kiza huwajui
Hodihodi waungwana, Nivalisheni kikoi
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai


Ya jana ndo ya ujana, Mzee sijisumbui
Hapo maisha hubana, Na kuhisi hupumui
Shida zikafumukana, Mithili utandubui
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai

Starehe za ujana, Mengi hauyang’amui
Hasa upatapo bwana, Hufanya hujitambui
Ila mtapotengana, Maziwa taona tui
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai

Ujana kubwa hazina, Kama mlima sinai
Ukicheza danadana, Hilo kosa la jinai
Mwisho chochote hakuna, Uzee utakudai
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai

Leo ilikua jana, Wakati hauzubai
Tumia vyema ujana, Dhalili nakupa rai
Ujana ulevi bwana, Uzee ni jitmai
Ya jana mpe kijana, Uzee asitumai

Tamati ninafikia, Mbele tena sisogei
Vyema ujana tumia, Afya isikulaghai
Usije ukajutia, Uzee ukisabai
Ya jana mpe kijana , Uzee asitumai

LIMETUNGWA NA NASRI KIONE
0752300012 nasriibrahimu@gmail.com
(FB) TUNGO ZENYE ULIMBO