Thursday, 28 May 2015

OA

OA

Oa nakwambia kaka, singoje kunasiwa,
Oa yapita miaka, ‘site ngoma kupigiwa,
Oa ‘epuke kumaka, usije kulia ngowa,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.


Oa walio na maadili, so sura kuangaliya,
Oa wenye uhiimili, epuka wenye umbeya,
Oa wenye muamali, nyumbani watatuliya,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa hata wa mjini, bora kwa mda kumjuwa
Oa aliye wa kuamini, sumu sije kutiliwa,
Oa kaka kwa makini, sije sema “ningejuwa,”
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa ukiwa kijana, ndoa mapema ku’ngiya,
Oa ulipe dhamana, vyema watoto kuleya,
Oa wajua ujana, ni moshi wa kufukiya,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa wakujitafutiya, nasaha yangu natowa,
Oa uliye dhamiriya, sio mke kuletewa,
Oa tena nakwambiya, sitake wakunadiwa,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa uepuke upweke, na msongo kujitiya,
Oa ukiwa na makeke, kabla uzee kuingiya,
Oa uhuni sitake, sije kufa kwa uthiya,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

Oa upate mwandani, kwa ubani kufukiwa,
Oa kitu cha dhamani, kinda bata na njiwa,
Oa na umweke ndani, waambiwe umeowa,
Oa uhisi mwenyewe, moyo utakavyopowa.

©2014 WILLY LUSIGE
"Malenga wa kuvizia"

SINA HAKI YA KUPENDA

SINA HAKI YA KUPENDA

Kwako mola shitakia, Dua zangu pokea,
Binadamu wachekea, umbile langu sikia,
Ufupi lonipatia, kunitusi wanambia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Ni majuzi litokea, kisa kilonifikia,
Mrembo alinambia, huba kwangu futilia,
 Weye nyundo sikia, kukupenda najutia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Mie ninazo hisia, kama warefu sikia,
Yarabi hakukosea, ufupi nakunumbia,
Mola unampangia, maumbile kashifia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Swali ninaulizia, malenga kunijibia,
Moyoni ninaumia, ninashindwa vumilia,
Matamshi lonambia, maulana nakwachia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Miaka imewadia, ninyi nyundo kubakia,
Twiga wameshaingia, naona mutaumia,
Ninaanza kujutia, ufupi livyonijia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Sio ninakwingilia, ukanamba nimevia,
Kiapo nakuapia, uliyanena sikia,
Rafiki sitokataa, japo mawi linambia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

Tamati Rama nalia, machozi yabubujia,
Nenda kwetu kutulia, dhiki imenivamia,
Yaillah yajalia, Jalie alo sawia,
Jamani mtu mfupi, hana haki ya kupenda?

RAMADHAN MWARUWA NYAE
“MALENGA MTI MGUMU”
MENZAMWENYE – LUNGALUNGA.